Ijumaa, 30 Januari 2015

PCT mafinga watumia mamilioni kusambaza mbegu kwa wakulima wa Pareto

Mkurugenzi  PCT Mafinga Mr. Martine Oweka

                                                      Shamba la Pareto....




KIWANDA cha Pareto (PCT), cha Mafinga wilayani Mufindi kimetumia zaidi ya shilingi milioni 350, kwa ajili ya kuwasaidia wakulima mbegu na miche ya zao hilo, ili kukuza na kuinua zao hilo.
Kila msimu wa Kilimo, kiwanda hicho kimekuwa kikisambaza mbegu na miche ya Pareto kwa wakulima wa zao hilo katika mikoa yote ambayo zao hilo limekuwa likistawi ikiwemo Iringa, Mbeya, Njombe na Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa kiwanda hicho Martine Oweka alisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha zao la Pareto ambalo ni mkombozi kwa mkulima.
Oweka amewataka wakulima wa mikoa hiyo    kulima zao hilo kwa wingi ili waweze kuinua kipato chao na kuondokana na umaskini kutokana na kuwepo kwa uhakika wa soko la zao hilo, tofauti na miaka ya nyuma kufuatia uwepo wa kiwanda.
Oweka alisema ili wakulima waondokane na umaskini, lazima wajikite katika mazao ya biashara likiwemo pareto, kutokana na zao hilo kwa sasa kuwa na bei nzuri katika soko la dunia.
 Alisema kuwa endapo wakulima wa mkoa wa Iringa na mingine inayostawisha zao hilo wataamua kulima pareto kama zao mama la biashara wanaweza kuondokana na umaskini, kutokana na ukweli kwamba, zoko la pareto limekuwa na uhakika tofauti na miaka ya nyuma wakati soko la zao hilo lilipoyumba.
Aliongeza kuwa kwa sasa kiwanda chao kinalima  zaidi ya ekari 300 za pareto, na kwamba kazi kubwa iliyopo ni kuhakikisha kuwa wakulima wanalima zao hilo na kufuatilia hatua zote za kupanda, kuvuna, kukausha na kusafirisha hadi kiwandani.

Akizungumzia masoko ya kimataifa Oweka alisema kuwa kwa sasa zipo nchi nyingi ambazo zinauhitaji mkubwa wa zao la pareto na ndiyo maana bei yake ipo juu.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Japani, India, Australia na nchi zilizopo bara la Ulaya kuwa wananunua pareto kwa wingi.

Mwisho.


Alhamisi, 18 Desemba 2014

JE WAIJUA MBEGU YA ZAO LA PARETO AINA YA MACHIPUKIZI?



Mbegu aina ya machipukizi hutokana na shina la zamani la pareto, shina hilo hung’olewa na baadaye huchanwa chanwa katika mche
moja moja na pasipo kuumiza mche.
 Ukisha andaa mbegu zoezi la kuandaa shamba na upandaji, linafuata. Shamba lilimwe vizuri kwa
kwa kuondoa magugu masumbufu kama Sangari. Matuta yenye sentimeta 60 toka tuta hadi tuta yaandaliwe.

Faida ya kutumia machipukizi ni
1. Mimea karibu yote hutoa maua kwa wakati mmoja
2. Ina kiwango cha juu cha sumu kwa kuwa mimea yote hufanana
3. Kipato cha maua makavu katika hekta ni kikubwa

Jumatano, 17 Desemba 2014

Je wajua namna ya kuandaa mbegu bora za Pareto?



ILI kupata Pareto bora na yenye kiwango na ubora unaotakiwa ili kukidhi mahitaji ya soko la dunia, ni  lazima kuwa na mbegu bora.
Namna ya kupata mbegu bora!
·     Chuma maua yaliyokomaa.
·     Kausha maua kwenye jua.
·     Piga maua ili kupata mbegu.
·     Pepeta ili kupata mbegu safi isiyo na pepe.
·     Andaakitalu cha mbegu na Otesha mbegu kwenye kitalu.
Mbegu huota baada ya siku 10-21, miche hukaa kitaluni kwa muda wa miezi 2-3 kisha huwa tayari kwa kupandwa.
Faida za kutumia mbegu halisi ni kwamba upatikanaji wake ni rahisi na kwamba Miche/mmea unaotokana na mbegu hizi hukua kwa nguvu sana.

Jumatano, 3 Desemba 2014

PATA UTANGULIZI KUHUSU PARETO NA MATUMIZI YAKE



Pareto iliingizwa na kuanza kulimwa kwa mara ya kwanza Tanzania mwaka 1931.
Zao hili la kibiashara hustawi vizuri katika Nyanda za juu za Tanzania.
Zao hili pia ni maarufu duniani kwa kuwa na maua yenye sumu aina ya kiua wadudu asili (Pyrethrins).
Sumu ya Pareto ina sifa kuu zifuatazo: Kuua wadudu kwa haraka baada ya kupata harufu yake; Inaua wadudu kwa jinsi ya pekee ikilinganishwa na sumu zinazotengenezwa viwandani;
 Haina athari kwa wanadamu katika matumizi yake; Ni rafiki wa mazingira kwa maana haiharibu mazingira ukilinganisha na zile za viwandani; Hairuhusu mdudu kujitengenezea uwezo wa kujihami.

Matumizi ya Pareto
Pareto hutumika kutengenezea madawa mbalimbali ya kuua wadudu. Makampuni ya madawa duniani hutumia sumu ya Pareto katika kutengeneza madawa,hilo ni moja.

Pili unga wa maua ya pareto hutumika kuhifadhi nafaka kama vile mahindi,maharage ili
yasishambuliwe na wadudu waharibifu.